Serikali imeahidi kuendelea kuandaa mazingira wezeshi, pamoja na kuharakisha uundwaji wa Sera na miongozo itakayosaidia wajasiriamali vijana, kuanza kunufaika na mpango wa upatikani mikopo kwa njia ya mtandao (Crowdfunding), pamoja na kuhakikisha fedha zitakazokusanywa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Hayo yameelezwa Dkt. Mursali Milanzi, mgeni rasmi, akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, wakati wa ufunguzi wa Warsa ya siku moja iliyoandaliwa na Chuo Kikuu Mzumbe, wakati wa kuwasilisha matokeo ya utafiti. Warsha hiyo ilifanyika katika ukumbi Royal Village, Dodoma na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka sekta ya fedha ikiwemo Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana.
Milanzi, amepongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa kubuni utafiti ambao utasaidia vijana kupata mitaji na kutatua changamoto kubwa ya mitaji kwa vijana, na kwamba utafiti huo utasaidia sana Serikali katika kuhuisha na kuandaa Sera na miongozi itakayotoa dira ya namna ya upatikanaji wa mitaji yenye riba na masharti nafuu, kwa makundi mbalimbali yaliyopo katika jamii kwa njia ya mtandao.
Akimkaribisha mgeni Rasmi, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha, amesema lengo la mradi huo ni kuelewa namna bora ya kukuza na kuendeleza biashara zinazoanzishwa na kuongozwa na vijana, kupitia upatikanaji wa mitaji ya ufadhili wa umati (Global Funding) kwa njia ya mtandao wa mawasiliano (internet), kuelewa tabia na vipaumbele vya wafadhili wa umati katika muktadha wa umbali mkubwa kijiongorafia, na tofauti za kitamaduni kati ya wahitaji wa mitaji na wafadhili wa mitaji, pamoja na kuelewa mikakati gani ni mizuri katika kuhakikisha vijana wa Kitanzania wananufaika na upatikanaji wa mitaji kupitia ufadhili wa umati kwa njia ya mtandao (internet), ambapo baadhi ya nchi za Afrika tayari zimeanza kunufaika na mpango huo.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, Mratibu wa Mradi huo Dkt. Nsubili Isaga, amesema mikoa iliyohusika katika utafiti huo ni Dar es salaam, Morogoro, Mbeya, Arusha na Mwanza, na matokeo ya awali yanaonesha idadi kubwa ya vijana hawatambui fursa hizo, wakati Utamaduni ukiathiri kwa sehemu kubwa uwepo wa utaratibu mzuri wa kuchangia maendeleo ya vijana kwa njia ya Umati.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mwakilishi kutoka Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha, Bi.Dionisia Mjema na Mwakilishi kutoka Soko la Mitaji, Bw. Charles Shirima, wamesema utafiti huo umekuja muda muafaka katika kuhakikisha soko la mitaji linakua na vijana wanatambua fursa mbalimbali zilizopo. Tayari hatua mbalimbali zimeshaanza kuchukuliwa na Serikali kwa kutunga Sera, Kanuni na Taratibu zinakazosaidia vijana wengi kunufaika na mpango huo pamoja na kujiepusha na makosa ya kimtandao ukiwemo wizi na utapeli.
Warsha hiyo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, Mashirika Binafsi na Taasisi ya Fedha yakiwemo Mashirika yanayojihusisha moja kwa moja na maendeleo ya Vijana.
Mradi unatekelezwa na Chuo Kikuu Mzumbe, kupitia Skuli ya Biashara, Idara ya Uhasibu na Fedha kwa ufadhili wa Serikali ya Denmark, kupitia "Danida Fellowship Centre”, na unategemewa kumalizika Januari 2024 Mradi huu.
******************************************